HATUA ZANGU CHUONI

Safari huanza kwa hatua moja baada ya nyingine, kutoka mwanzo hadi kileleni. Safari hueza kuzongwa na milima na mabonde. Uvumilivu, bidii pamoja na matumaini humwezesha yeyote kukamilisha safari yake. Haijalishi ni safari gani, safari yoyote yaeza kuwa ya kawaida, kutoka eneo moja la kijiografia hadi linguine au safari ya hali ya kimaisha.

Kama himizo kwa kila mtoto yeyote anayezaliwa duniani, nia ya wazazi wake ni kumlea vyema, kwenye maadili mazuri na zaidi kuimarisha ukuzi wake na zawadi ya elimu ya kimaisha na darasani. Pindi unapoianza safari hii kwenye hatua ya chini, shule ya chekechea tumaini la mzazi ni  mtoto wake kufika kileleni mwa masomo yake. Kilele chake kikiwa chuo kikuu na kusomea taaluma bora zenye thamani.

Kwenye makuzi yangu ningali mdogo shule ya msingi ya Brainsgate nilikuwa na lengo la kujiunga na chuo kikuu na kujikita na taaluma ya uanahabari. Nilijizatiti na kujitahidi masomoni na hatimaye ndoto yangu ilitimia na kuamka nikiwa chuo kikuu cha kiufundi Cha Mombasa. Taaluma ikiwa ile ya utotoni ya kuwa mwanahabari.

Nilijiunga na chuo hiki na kuzamia kwenye taaluma ya miaka mitatu. Safari iliyojaa milima mingi na mabonde mengi, nikimwomba Mola anijalie nguvu na uwezo wa kukamilisha taaluma hii vyema. Kadri masomo yalikuwa yakinoga, miaka ndivyo ilikuwa inasonga, umri nao haukuchelea kujikuza. Mabadiliko yalidhihirika si kwenye ukuaji pekee bali pia kuimarika kwa kufanya maamuzi na kutofautisha lipi bora na lipi baya aghalabu kila hatua ilitangulizwa kwa dua za Mola.

Vyuo vikuu huwa na sifa nzuri pamoja na sifa mbaya. Mwanafunzi anaeza potoka na pia anaeza kujengeka bora. Mwaka wangu wa kwanza shuleni nilijizatiti nisivuliwe na vijana wapotofu wenye maadili mabaya. Nilijitahidi nisijihusishe na hatua mbaya kama kuvuta bangi, kula unga, kujihusisha na wizi pamoja na usherati. Masomoni nilijizatiti kutimiza ahadi nilizowapatia wazazi za kuwa kinara darasani kila wakati. Hii iliwapa furaha na kuwatia motisha na kujitolea kwa hali na mali kunisomesha bila ugumu wowote. 

Comments

  1. This comment has been removed by the author.

    ReplyDelete

Post a Comment

Popular Posts